Pages

Tuesday, February 22, 2011

JANUARY MAKAMBA: Dalali au Mzalendo?

 
hii nimeitoa raia mwema


JANUARY MAKAMBA: Dalali au Mzalendo?



Msomaji Raia Februari 16, 2011









SHIDA haina adabu. Yaweza kumfanya nyang’au kuwa mzalendo na mzalendo kuwa nyang’au. Mbunge wa Bumbuli, Mheshimiwa January Makamba, wiki iliyopita alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini ndani ya bunge letu tukufu.



Si bahati mbaya kwa January kuchaguliwa katika kamati hii. Ni mpango mahsusi tena ulioratibiwa kwa umakini mkubwa na kundi lenye nguvu na jeuri ya fedha katika taifa letu. January anaweza kuwa anaujua mpango huu, au ameshirikishwa katika hatua za mwisho.



Itakumbukwa kamati hii nyeti ya bunge, katika bunge lililopita, iliongozwa na Mzee Shelukindo aliyekuwa mbunge wa Bumbuli. Kilichofanyika sasa ni kama January Makamba ‘amerithishwa’ kila kitu cha Mzee Shelukindo; yaani jimbo, kiti katika ukumbi wa bunge na kamati aliyoiongoza Mzee Shelukindo.



Kwa tulioshuhudia mchakato mzima wa uchaguzi, tuna haki ya kusema kuwa huu si mpango wa kurithishana bali ni mwendelezo wa mapinduzi yasiyo na damu yaliyoratibiwa na kundi la mafisadi ambao ni wazi sasa limetanda kila kona ya nchi na kujiimarisha katika vyombo vyote muhimu vya maamuzi ya taifa letu.



Kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge, January Makamba alikuwa Ikulu akimsaidia Rais Kikwete kama mwandishi wa hotuba. Ni kijana anayesemekana kuwa jasiri na mwerevu, lakini lililo la muhimu ni ukweli kuwa anajisikia na kukiri kuwa ni mwerevu, jasiri na asiyeshindwa kirahisi.



Baba yake Mzee Makamba anamnadi kila mahali kuwa ni kijana mwenye akili nyingi, na siku za karibuni Mzee Makamba amevunja ukimya mbele ya marafiki zake na kumlaumu Rais Kikwete kwa kushindwa kutimiza ahadi yake ya kumpa mwanae uwaziri. Mzee Makamba amefikia hatua ya kujuta kuwa nafuu kijana wake angebaki Ikulu kuliko kuwa mbunge bila kuwa waziri. Silaha ya Rais Kikwete kutuliza mizuka ya namna hii huwa ni kutoa ahadi, na safari hii amemuahidi kuwa atampa wizara atakapofanya mabadiliko ya baraza la mawaziri siku chache zijazo!



Taifa letu linakabiliwa na uhaba mkubwa wa nishati ya umeme. Upungufu huu umesababisha kero kubwa kwa njia ya migawo ya umeme isyokuwa na utaratibu maalumu. Kazi maofisini na viwandani haziendi na dalili za uchumi kudorora ziko wazi.



Hali hii imelifikisha taifa katika njia panda ya ajabu. Kwamba, tatizo hili ambalo katika hali ya kawaida lingetatuliwa na serikali, sasa linadaiwa kuhitaji nguvu ya bunge ili kuweza kulitatua. Hakuna anayejiuliza endapo bunge litashindwa kama lilivyoshindwa mengine, ni nani tena ataweza?



Mantiki inaweza kutaja mhimili wa mahakama au jeshi kwa kuwa ndivyo vyombo vilivyobaki katika kutatua matatizo yaliyoshindikana kama hili.



Ni uzembe wa hali ya juu kukubaliana na ukweli kwamba serikali inashindwa kutatua suala la kawaida kama hili na kulazimisha bunge ndilo liingie kutafuta suluhisho lake. January Makamba amedai ikibidi “ataishinikiza” serikali kupata suluhisho la mgawo wa umeme nchini.



Ikiwa hili litawezekana, tutapata fundisho kuwa, kwa njia ya mashinikizo, suluhu ya matatizo sugu ya taifa letu inaweza kupatikana. Kwa njia hiyo basi, serikali hii ishinikizwe kutatua hata matatizo mengine yaliyo sugu katika taifa letu!



January Makamba anadai siasa ndiyo imepeleka nchi gizani. Anamsuta Waziri wa Nishati na Madini kuwa aache kuorodhesha miradi ya uzalishaji umeme kwa sababu kinachohitajika ni umeme si orodha ya miradi. Tumewahi kusikia kauli kama hizi siku za nyuma pale kundi fulani la wanasiasa walipokuwa wanashinikiza taifa lifunike kombe ili mwana haramu aweze kupita.



Jitihada za kutatua tatizo la umeme zilijaa kila aina ya ufisadi na kwa kuwa wananchi wanataka umeme, basi, wakawa wanashinikizwa wakubali ufisadi ili wapate umeme. Jitihada hizo ziliposhindwa, likatolewa tishio kuwa taifa litakapoingia gizani, ndipo tutakapojua gharama za kuendekeza siasa.



Nadhani lile halikuwa tishio; maana sasa ni dhahiri kuwa taifa liko gizani, na January Makamba anakuja na suluhisho mfukoni ili kutuondoa gizani. Tuombe Mungu isije kuwa ni kwa gharama za Taifa kukubaliana na masharti ya mafisadi.



Mabwawa ya maji yanaelekea kukauka; mitambo ya kigeni (IPTL) inayozalisha umeme inatumia mafuta mengi sana na kiwango cha uzalishaji hakitoshelezi mahitaji. TANESCO inakabiliwa na faini ya Sh. bilioni 94 kwa kuvunja mkataba na Dowans. Mitambo ya Dowans iko Ubungo na ina uwezo wa kuzalisha nishati inayohitajika. Kuilipa Dowans bila kuweka mkataba mpya nayo ili izalishe nishati hiyo hakutaliondoa taifa gizani.



Kwa kifupi, Taifa liko njia panda, na linahitaji kufanya uchaguzi kati ya kuwaabudu mafisadi na kupata umeme au kukataa na kubaki gizani kwa muda. January Makamba ameahidi kuongoza kamati yake katika kuisimamia serikali na kuhakikisha nishati inapatikana.



Kimsingi, January Makamba anasema wazi kuwa serikali imeshindwa na sasa inahitaji utashi wa kibunge ili kutatua tatizo hili. Wengi tumekuwa tukichambua ombwe la uongozi wa taifa letu, na hapa tuna mtu aliyetokea jikoni akiwa na njia mpya ya kutatua tatizo la umeme!



January Makamba anaweka hoja mezani kuwa mitambo ya Dowans iwashwe kwa mkataba wa muda wakati kesi yake inaendelea mahakamani. Ikibidi fedha zinazopatikana ziwekwe katika mfuko maalumu kusubiri kesi iliyo mahakamani. Rais Kikwete amekuwa akisema wazi kuwa hapendi serikali yake kuingilia uhuru wa Mahakama.



Naamini si vema pia Bunge kuingilia uhuru wa Mahakama. Ni kitu gani kinamfanya January Makamba afikiri anao ushawishi, nguvu na hekima mpya iliyokosekana huko nyuma hadi nchi ikaingia gizani? Katikati ya harakati hizi, yapo madai kuwa January Makamba anakuja na pendekezo alilopewa na mafisadi kuwa, Dowans wapunguze au kusamehe deni wanaloidai TANESCO lakini nao wapate mkataba wa kuzalisha umeme kwa muda usio na ukomo.



Nimesema kuwa hayo ni madai, lakini kama itabainika kuwa kweli, basi, lugha yake ya kizalendo itageuka kuwa ya kidalali na isiyo ya kizalendo. Wakati hakuna bei itoshayo kununua uzalendo, lakini tuna hakika kuna bei ya udalali, na ni wenyewe Dowans wanaojua wametenga kiasi gani cha fedha kunadi mitambo yao ndani ya Bunge na Serikali.















msomajiraia@yahoo.co.uk

No comments: