Mussa Juma, Loliondo na Deusdedit Moshi, Dodoma
DAKTARI Joachiam Mbosha wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Ngorongoro ya Wasso, amethibitisha kuwa mmoja wa wagonjwa wa Ukimwi aliyekwenda kutibiwa kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapile, maarufu kwa jina la 'Babu', huko Samunge, Loliondo amepona Ukimwi.
Wilia John Lengume (30), juzi alikuwa kivutio kwa mamia ya watu baada ya kutangazwa na Mchungaji Mwasapile kwenye ibada iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Sonjo iliyoshirikisha mamia ya watu. Akizungumza katika ibada hiyo, Mchungaji Mwasapile alisema Lengume ndiye aliyekuwa mgonjwa wa kwanza kumtibu.
Akizungumza na Mwananchi kanisani hapo, Lengume alisema baada ya mumewe, John Meneyi Lengume kufariki dunia mwaka 2002, aliamua kwenda kupima na kuonekana kuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) lakini baada ya kutumia dawa hiyo alisema sasa hana tena virusi vya Ukimwi. Alisema kwa muda mrefu mama huyo alikuwa akitumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARV) katika Kituo cha Afya Didodigo wilayani Ngorongoro.
Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu kupona kwa mama huyo, Dk Mbosha alisema: “Hiki kitu kilituchanganya sana, nakumbuka mimi ndiye nilimpima mwaka jana... ikabidi niwaeleze watu wa maabara Hospitali ya Wasso ili wafuatilie aliyempima awali huyu mama na nilimweleza aache kutumia dawa kwani hana HIV,” alisema Dk Mbosha.
Dk Mbosha alisema alihamishiwa katika kituo hicho cha Afya cha Digodigo zaidi ya mwaka mmoja uliopita na alimkuta mama huyo akiendelea kuhudhuria kliniki na kupata ARV pamoja na ushauri wa kulinda afya yake lakini alianza kuona mabadiliko makubwa ya afya yake na ndipo alipoamua kumpima tena.
Aliamua kumpima mwaka jana baada ya kuona 'CD4' (kinga za mwili) zake zinaimarika kiasi cha kutohitaji kuendelea kutumia dawa hizo za kupunguza makali.Aliamua kumhoji kujua siri iliyokuwa imejificha katika mabadiliko hayo ambayo alisema yalikuwa ya haraka haraka mno na ndipo alipomweleza kwamba alipata tiba kutoka kwa Mchungaji Mwasapile.
Lengume alisema licha ya mumewe kufariki, mtoto wao mmoja pia alifariki dunia lakini baada ya kutumia dawa ya Mchungaji Mwasapile, maisha yake ni mazuri na ana mtoto mwingine mchanga anayeitwa Evelyn ... “Namshukuru Mungu na Mchungaji Mwasapile sasa nimepona na ninaishi maisha mazuri tu.”Alisema baada ya kuanza kuugua, mchungaji huyo, ndiye aliyemfuata na kumuomba amtibu akimthibitishia kwamba atapona maradhi yaliyokuwa yakimsibu.Hata hivyo, kitalaamu bado haijathibitika kupatikana kwa tiba wala chanjo ya Ukimwi.
Ushuhuda wa Mzee Mtaki
Mwingine aliyejitangaza kupata ahueni kubwa kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsibu baada ya kupata tiba ya mchungaji huyo ni aliyewahi kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Mzee Ali Said Mtaki.Mzee Mtaki (81) ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Mpwapwa katika miaka ya 1980, Mkuu wa Mikoa ya Dodoma na Singida kwa nyakati tofauti, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mbunge wa Afrika Mashariki na kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Usharika Mkoa wa Dodoma, alikuwa anasumbuliwa na matatizo ya kutetemeka kiasi cha kushindwa kutembea na kuzungumza vizuri.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Mtaa wa Nyerere Mjini Dodoma, Mzee Mtaki alisema tangu anywe dawa ya mchungaji huyo Jumanne ya wiki iliyopita huko Loliondo, sasa anaendelea kupata nafuu siku hadi siku.
Akiongea kwa kujiamini alisema sasa anajiona kama amepona na anaweza kuendelea na shughuli zake ikiwamo ya uwakala wa bima... "Si unaona nilikuwa natembea kwa shida, kuzungumza kwa taabu, sasa hali yangu ni nzuri nafanya kila kitu bila kusaidiwa.”Akielezea safari yake ya siku mbili ambayo ilimfikisha kijijini Samunge, Loliondo anasema alifuatana na mkewe, Amina Mtaki ambaye naye alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na mgongo. Anasema naye pia amepona.
Anasema safari ya kutoka Dodoma hadi Samunge iliwagharimu Sh60,000 kila mmoja na baada ya kufika huko walikuta umati mkubwa wa watu ukisubiri kupata tiba hiyo. Anasema aliwakuta watu wa mataifa mbalimbali, Waafrika, Wahindi, Wazungu na Waarabu... "Watu walikuwa wengi na kila mtu na matatizo yake lakini Mchungaji alikuwa akiwasisitizia kwamba habagui watu na haangalii dini au uwezo wa mtu."
“Katika mkusanyiko huo nilibahatika kukutana na Askofu Thomas Laizer wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati akiwa amefuatana na mama wa kizungu. Nilikaa karibu na mama yule wa kizungu ambaye sikumbuki jina lake. Nilimshika Askofu Laizer mkono tukasalimiana na kuongozana naye kuelekea kwa Mchungaji Ambilikile."
"Tulipofika kwa Mchungaji, Askofu Laizer akamwambia mchungaji kwamba ana wageni wake, hivyo mama yule wa kizungu akapewa dawa na mimi pia nikapewa na mke wangu akapewa pamoja na kijana wangu japo yeye hakuwa na tatizo lolote la kiafya."
No comments:
Post a Comment