Pages

Wednesday, March 16, 2011

Serikali, Ndesamburo watimiza ahadi Loliondo

Monday, 14 March 2011 21:37

0diggs

digg

Wananchi mbalimbali wa mji wa Moshi na vitongoji vyake wakijiandikisha katika ofisi za Mbunge wa Jimbo la Moshi mjini, Philemon Ndesamburo kwa ajili ya kwenda Loliondo kupata tiba ya dawa kwa mchungaji Ambilikile Mwasapile. Picha na Dionis Nyato

Waandishi Wetu

SERIKALI imeanza kutimiza ahadi yake ya kumsaidia Mchungaji Ambilikile Mwasapile (76) anayedaiwa kutoa tiba ya magonjwa sugu katika Kijiji cha Samunge, Loliondo, mkoani Arusha baada ya kutoa mashine ndogo ya kufua umeme (jenereta) na kupeleka wauguzi na askari wa kutosha.



Wiki iliyopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema Serikali ilikuwa inaandaa utaratibu wa kutuma idadi ndogo ya wauguzi ambao wangesaidia kutoa huduma kwa watu watakaohitaji ambazo zingekuwa nje ya zile zinazotolewa na Mchungaji Mwasapile. Aliahidi kupeleka gari la kubebea wagonjwa (ambulance) kijijini humo ili kutoa msaada wa haraka kwa watu watakaohitaji huduma hiyo.



Kutokana na mchango huo, kazi ya ugawaji wa dawa hiyo kuanzia juzi ilikuwa ikienda kwa haraka zaidi tofauti na awali. Pia sasa wagonjwa mahututi wanafikishwa kwanza kwa wauguzi kabla ya kupelekwa kwa mchungaji huyo Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).Pia Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wameweka kambi jirani na nyumba za Mchungaji Mwasapile na wamekuwa wakisimamia magari na hata kusaidia kusambaza vikombe vya dawa kwenye magari hayo ili kuondoa msongamano.



Aidha, kupatikana kwa huduma hiyo ya umeme, hivi sasa Mchungaji Mwasapile ameanza kufanya kazi hadi usiku, kutokana na Serikali kupitia Halmashauri ya Ngorongoro, kumkabidhi jenereta hiyo. Sasa inasaidia kupatikana kwa mwanga wa kutosha katika eneo analotoa tiba na nyumbani kwake.



“Naishukuru sana Serikali kwa kuleta umeme hapa na kuna wauguzi wamekuwa wakisaidia watu wanaokuwa mahututi, ila bado kuna tatizo la vyombo vya kuchemshia na kutolea dawa kutokana na ongezeko kubwa la watu,” alisema Mchungaji Mwasapile.Mwenyekiti wa Kijiji cha Samunge, Michael Lengume alisema tayari Serikali ya Kijiji hicho kwa kushirikiana na viongozi wengine wameunda kamati mbalimbali za kukabiliana na wingi wa watu.



“Kijiji chetu kina kaya 500, sasa. Wingi wa watu ambao unafikia hadi 30,000 kwa siku ni janga na ndiyo sababu tumejipanga kuhakikisha hakuna madhara ambayo yanatokea,” alisema Lengume na kutaja moja ya kamati hiyo kuwa ni ya afya, usafi na mazingira.“Pia tumehamamisha watu kuleta vyakula hapa na huduma nyingine na sasa chakula kipo. Hakuna sababu mtu kutoka Dar es Salaam kuja na chakula chake,” alisema Lengume.



Alitoa wito kwa kampuni za simu kupeleka minara ya mawasiliano japo ya muda ili kuondoa adha ya watu kukosa mawasiliano na ndugu zao wakiwa kijijini hapo.Mwandishi wa habari hizi juzi aliwashuhudia wauguzi wakiwabeba wagonjwa kwenye machela na kuwapeleka kunywa dawa kwa mchungaji Mwasapile na baadaye kuwabeba na kuwarejesha katika Zahanati ya Samunge kupumzika.



Tatizo kubwa sasa ni jinsi ya kufika kwa mchungaji huyo na kuna wasiwasi kwamba kama mvua zikiendelea kunyesha itakuwa vigumu kwa wananchi kufika huko kupata huduma. Tatizo ni kubwa hasa kwa wananchi wanaotumia Barabara ya Kigongoni, Engaruka, pembezoni mwa Mlima Oldonyolengai, Digodigo hadi kufika Samunge.



Akizungumza kwa simu kutoka Arusha baada ya kutoka Semunge kupata matibabu, mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Stella Ludovick alisema pamoja na misaada mingine ya kibinadamu, ujenzi wa barabara ya kuelekea katika kijiji hicho ni muhimu zaidi."Ndiyo, misaada hiyo mingine ni muhimu lakini, barabara ni tatizo la msingi kabisa. Serikali inapaswa kulishughulikia haraka tatizo la barabara kama kweli ina nia ya kusaidia huduma ya babu huyo," alisema Stella.



Alisema ilimchukua saa tisa kutoka Arusha hadi kijijini Semunge... "Barabara ni mbaya sana na kimsingi hili ndilo tatizo kubwa. Sisi tuliondoka Arusha saa 4:00 usiku na kufika kijijini huko saa 3:00 asubuhi ya siku iliyofuata. Saa tisa mtu uko njiani."Magari yanayotumika ni magari ya watalii ambayo mvua ikinyesha, hayawezi tena kwenda.



Nauli yake kutoka Arusha hadi Loliondo ni Sh150,000 kwa abiria. Zamani magari hayo yalikuwa yakisubiri abiria lakini kutokana na msongamano wa wagonjwa hili limekuwa haliwezekani tena. Mfanyabiashara gani atasubiri juma moja kupata tiba?"



Alisema maeneo mengi ya barabara hiyo ni mabaya kutokana na kujaa vumbi na mashimo, huku wingi wa magari yanayosafirisha wagonjwa kuelekea katika kijiji hicho yakiongeza tatizo hilo.



Ndesamburo atimiza ahadi

Mbunge wa Moshi Mjini, Phillemon Ndesamburo ametimiza ahadi ya kutoa usafiri bure kwa wakazi wa jimbo hilo kwenda Loliondo kwa Mchungaji Mwasapile.Ndesamburo aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tangu kuanza kwa huduma hiyo amegundua kuwa wananchi ndiyo wanaopata shida zaidi kufika Loliondo.



Alisema baada ya kuguswa na tatizo hilo, ametoa magari mawili aina ya Bedford na Youmork yenye uwezo wa kubeba wagonjwa 73 ambayo yataanza kutoa huduma kesho. Hata hivyo, Ndesamburo alikuwa ameahidi kuwapeleka wananchi wa jimbo lake huko Loliondo kwa helikopta yake kabla ya kubadili uamuzi huo na kutumia magari hayo makubwa.



Alisema msaada huo hauhusiani na itikadi za chama cha siasa. Usafiri huo ni kwa ajili ya wakazi wa Moshi Mjini na vinatumika vitambulisho vya kupigia kura kuwabaini.Ndesamburo alifafanua kuwa wakazi hao watatakiwa kujitegemea chakula, maji na Sh500 ya kumlipa mchungaji huyo.



Mbunge huyo alisisitiza kuwa huduma hiyo si ya muda mfupi hivyo kuwatoa wasiwasi wakazi ambao wamekuwa wakigombea kwenda katika awamu ya kwanza kwa hofu kuwa inaweza iwe ndiyo mwisho.

Habari hii imeandikwa na Kizitto Noya, Dar; Mussa Juma, Loliondo na Fina Lyimo, Moshi.

No comments: