Tuesday, 22 March 2011 20:42
Mussa Juma, Arusha na Dotto Kahindi
SERIKALI imewataka watu wanaowapeleka wagonjwa kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapile kupata tiba ya magonjwa sugu kuacha kufanya hivyo kwa muda kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kuharibu barabara ya kwenda Loliondo.
Imesema kwamba kuendelea kuongezeka kwa watu wanaokwenda huko wakiwa wagonjwa kutasababisha vifo kwa sababu magari mengi yanakwama barabarani maeneo ambayo hakuna huduma za vyakula, maji na dawa.
Kutokana na uamuzi huo na hali halisi ya barabara ya kufika huko, baadhi ya wananchi wamemwomba mchungaji huyo kuhamia jijini Arusha ili kuepusha madhara ambayo yanawakabili watu wanaohitaji huduma yake.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore Shirima alisema Serikali haina nia ya kuwazuia watu kwenda kupata matibabu lakini mazingira yaliyopo sasa kuelekea katika Kijiji cha Samunge aliko Mchungaji Mwasapile, si mazuri.
"Naomba watu watuelewe, Serikali haina mpango wa kuwazuia kwenda kupata matibabu kwani suala hili ni la kiimani, lakini tunaomba watuelewe kuwa sasa hali si nzuri (kijijini) Samunge," alisema Shirima.
Alisema haitakuwa rahisi watu wanaokwenda sasa Samunge kupata huduma muhimu kama chakula, vinywaji na mahitaji mengine na wakati mwingine itawabidi kutembea kwa miguu kilomita 20 ili kufikia huduma hiyo.
Alisema katika kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa, ofisi yake imewasiliana na mikoa ya jirani ili watu wapewe elimu zaidi kuepuka athari zinazoweza kuwapata... "Sasa hali si nzuri. Tunaomba watuamini na hali ikiwa nafuu hasa kutokana na foleni ya magari, tutatoa taarifa."
Alisema Serikali inatarajia kukutana na Mchungaji Mwasapile ili kuweka utaratibu mzuri wa kutoa tiba hiyo kulingana na idadi ya watu.Wakati huohuo; Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa kushirikiana na wasafirishaji wa abiria kwenda Samunge, wameanza kuweka utaratibu wa kusimamia magari yanayokodiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye alisema jana kuwa utaratibu unaandaliwa wa kuratibu magari yote yanayokwenda Loliondo kutoka Arusha katika kituo maalumu. Hiyo imetokana na kuwapo kwa taarifa kwamba kuna magari yanayowatapeli abiria na kuwatelekeza njiani baada ya kuchukua fedha.
Mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji ya Shufaa ambayo hupeleka watu Loliondo, Saidi Kakiva alisema wamekubaliana kusajili magari yote ambayo yanakwenda Loliondo.
“Kumeibuka tabia ya kutelekeza wagonjwa na wengine kutupwa porini, hasa wale wanaofariki, hivyo sasa magari yanaandikwa namba na madereva wanaandikwa majina ili kuwadhibiti,” alisema Kakiva.
Kuhusu ombi la kumtaka Mchungaji Mwasapile ahamishie huduma zake Arusha, baadhi ya ndugu na jamaa za wagonjwa waliokwama katika barabara iendayo Samunge, wamesema hilo linaweza kuwa katika kipindi hiki ambacho barabara ya kwenda nyumbani kwake imeharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Mmoja wa wananchi hao, Josephat Mwangoka anayetokea Dar es Salaam akimpeleka baba yake mzazi alisema: “Tunamuomba sana Mchungaji ahamishie shughuli zake walau Arusha mjini ili watu waweze kumfikia kwa urahisi hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zimeharibu barabara. Hivi sasa watu wanatumia gharama kubwa mno kwenda kumuona kutokana na matatizo ya barabara.”
source:mwananchi communication
No comments:
Post a Comment