Pages

Monday, February 28, 2011

Uthibitisho wa Mhe. Lema kuhusu Pinda kuongea uongo Bungeni


Maelezo ya uthibitisho ya Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema (mbunge) juu ya kauli ya uwongo iliyotolewa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo P.K. Pinda (mbunge) wakati akijibu maswali kwa Waziri Mkuu katika kikao cha tatu cha mkutano wa pili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tarehe 10 Februari, 2011Mheshimiwa Spika,Kwa mujibu wa Hansard ya tarehe 10 Februari 2011, nilikuomba “kupata ufafanuzi kwamba Mbunge anaweza akachukua hatua gani kama anaona mtu mwenye nafasi kubwa katika nchi kama Waziri Mkuu analidanganya taifa na kulidanganya Bunge.” Badala ya kunipatia ufafanuzi niliouomba, Mheshimiwa Spika ulitoa kauli ifuatayo, kwa mujibu wa Hansard hiyo: “Mheshimiwa Mbunge, Bunge hili lazima liwe na adabu inayostahili. Kwa hiyo kama tutafanya Bunge letu hili ikawa ni mahali, sasa unataka kusema Waziri Mkuu kwa ahadi aliyoweka ndani ya Bunge hili anadanganya? Kama anadanganya naomba ukaiandike vizuri kabisa kuhusu kudanganya kwake, halafu nitakuambia tufanye nini.”Mheshimiwa Spika,Baada ya maelekezo hayo ya awali, ulitoa maelekezo ya ziada kwamba “nampa mpaka tarehe 14 asubuhi alete maandiko ya kuthibitisha maneno aliyoyasema…. Kwa hiyo tarehe 14 kipindi cha asubuhi atoe maelezo ya kwamba Waziri Mkuu amesema uongo. Maana yake alichosema kwamba Waziri Mkuu amesema uongo sasa anataka tumpe Mwongozo wa namna ya kufanya na akasema aandike. Sasa kifungu hiki cha 64 kinamdai alete maelezo hayo mpaka tarehe 14.”Mheshimiwa Spika,Maneno yote ya Hansard niliyoyanukuu hapo juu yanathibitisha kwamba mimi sikusema Waziri Mkuu amesema uongo, bali niliomba mwongozo wa Spika kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa na Mbunge endapo kiongozi wa ngazi za juu kama Waziri Mkuu atasema uongo au kulidanganya Bunge. Hata hivyo, kwa vile umenielekeza nitoe maelezo uthibitisho kwamba Waziri Mkuu alisema uongo au kulidanganya Bunge, na kwa kutimiza maelekezo yako, naomba sasa nithibitishe kwamba kauli ya Waziri Mkuu kuhusu matukio yaliyopelekea mauaji ya wananchi wa Arusha na Mbarali yalikuwa ya uongo na kwamba Waziri Mkuu alilidanganya Bunge.1. UONGO WA KWANZA

Mheshimiwa Spika,Waziri Mkuu amenukuliwa kwenye Hansard ya tarehe 10 Februari 2011 akidai kwamba “… tumepoteza maisha ya Watanzania watatu bila sababu.” Huu ni uongo wa kwanza wa Waziri Mkuu Bungeni. Ukweli ni kwamba waliopoteza maisha ni Watanzania wawili – Dennis Michael Shirima na Ismail Omari – na Mkenya mmoja aliyejulikana kwa jina la Paul Njuguna.2. UONGO WA PILI

Mheshimiwa Spika,Kwa mujibu wa Hansard ya tarehe 10 Februari 2011, Waziri Mkuu alitamka maneno yafuatayo kuhusu suala la maandamano ya Arusha: “Mliomba wenyewe mfanye maandamano, hatukukataa, mkakaa na askari pale mkaelewana vizuri. Mkakubaliana kwamba sisi tunafikiri ili tuweze kuwadhibiti vizuri na kuwalinda vizuri, tutumie route moja tu. Wenzangu nyie mkakataa.” Kauli mbili za mwisho kwamba zina maana kwamba Jeshi la Polisi lilipendekeza kwamba njia moja ya maandamano ndiyo itumike na kwamba viongozi wa CHADEMA walikataa pendekezo hilo. Kauli hiyo, Mheshimiwa Spika, ni ya uongo na ilikuwa na lengo la kulidanganya Bunge.Mheshimiwa Spika,Ukweli wa jambo hili ni kwamba tarehe 31 Desemba 2010, Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Arusha Mjini alitoa taarifa ya maandishi kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha Mjini yenye kumb. Na. CDM/AR/W/20/10 yenye kichwa cha habari: “TAARIFA YA MAANDAMANO NA MKUTANO WA HADHARA TAREHE 5 JANUARI 2011.” Sehemu ya barua hiyo ilimjulisha Mkuu wa Polisi wa Wilaya kwamba “… CHADEMA (Wilaya ya Arusha Mjini) tutakuwa na maandamano ya amani tarehe 5 Januari 2011 yatakayohitimishwa na mkutano wa hadhara katika viwanja wa NMC – unga Ltd.” Aidha, barua hiyo ilipendekeza njia ifuatayo ya maandamano hayo: “Maandamano hayo yataanzia maeneo ya Phillips saa NNE asubuhi, kuelekea Sanawari, Mianzini, Stand Kuu kuelekea Mnara wa Azimio, kupitia Polisi – Manispaa – Clock Tower kushukia Sokoine Road, kasha Friends’ Corner na kuingia viwanja vya NMC.” Nakala ya taarifa hiyo ya CHADEMA kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Arusha Mjini imeambatanishwa katika maelezo haya kama Kielelezo ‘A.’Mheshimiwa Spika,Mnamo tarehe 2 Januari 2011, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Arusha Mjini alimwandikia Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha Mjini barua nyingine yenye kumb. Na. CDM/AR/W/20.1/11 ambapo alimjulisha kwamba “msafara wetu utabaki kama tulivyoainisha kwenye barua (ya tarehe 31 Desemba 2010.)” Vile vile barua hiyo ilimjulisha Mkuu wa Polisi wa Wilaya juu ya “… vituo maalumu vya wananchi kukutana ili baada ya hapo waweze kujiunga na maandamano (msafara mkuu).” Nakala ya barua ya tarehe 2 Januari 2011 nayo imeambatanishwa kama Kielelezo ‘B’ kwenye maelezo haya.Kwa ushahidi huu wa maandishi, ni wazi kwa hiyo kwamba kauli ya Waziri Mkuu kwamba Jeshi la Polisi la Wilaya ya Arusha Mjini ndio waliopendekeza njia ya maandamano ilikuwa ni ya uongo na/au ililenga kulidanganya Bunge.Mheshimiwa Spika,Mnamo tarehe 3 Januari 2011 viongozi wa CHADEMA wa Wilaya ya Arusha Mjini walikutana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha ili kujadili masuala mbali mbali yanayohusu maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 5 Januari. Moja ya mambo yaliyojadiliwa katika mkutano huo ndani ya Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa ilikuwa ni kuchagua njia muafaka zaidi ya maandamano hayo. Kufuatia mazungumzo hayo, mnamo tarehe 4 Januari 2011 Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha SSP Zuberi Mwombeji alimwandikia Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Arusha Mjini kumjulisha kwamba “kimsingi mmekubaliwa kufanya maandamano na mkutano wenu wa hadhara tarehe 5 Januari 2011….”Katika barua hiyo, Mkuu wa Polisi aliitaka CHADEMA ichague moja kati ya njia mbili za maandamano ambazo zilijadiliwa na kukubaliwa katika mkutano wa tarehe 3 Januari, yaani njia ya “kuanzia Phillips, Sanawari Mataa, kushuka na barabara ya AICC, Goliondoi, Sokoine Road, Friends Corner na kuingia uwanja wa NMC”; au “kuanzia Phillips, sanawari Mataa, Mianzini Mataa, Florida Annex, Stand, CRDB Bank, Friends’ Corner hadi uwanja wa NMC.” Nakala ya barua ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya yenye kumb. Na. AR/B.5/VOL.II/63 imeambatanishwa kama Kielelezo ‘C’ kwenye maelezo haya. Siku hiyo hiyo ya tarehe 4 Januari 2011 Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya alimtaarifu Mkuu wa Polisi Wilaya kwamba maandamano yangepitia njia ya Phillips, Sanawari Mataa, Mianzini Mataa, Florida Annex, Stendi Kuu ya Mabasi, CRDB Bank, Friends’ Corner na kuingia viwanja wa NMC – Unga Ltd.Kufuatana na mtiririko huu wa matukio, sio kweli kwamba Polisi ndio waliopendekeza njia ya maandamano na wala sio kweli kwamba CHADEMA walikataa njia hiyo iliyopendekezwa na Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, kauli ya Waziri Mkuu Bungeni kwamba Polisi walipendekeza njia ya maandamano na CHADEMA wakaikataa ilikuwa ni kauli ya uongo na yenye lengo la kulidanganya Bunge.3. UONGO WA TATU

Mheshimiwa Spika,Aya ya tatu ya kauli ya Waziri Mkuu inadai kwamba Jeshi la Polisi lilizuia maandamano ya CHADEMA kihalali lakini CHADEMA wakaamua “… kufanya maandamano yale bila kujali kabisa kwamba utaratibu uliokuwa wamekubaliana mmeukiuka wenyewe.” Kauli hii ya Waziri Mkuu ni ya uongo na ilikuwa na lengo la kudanganya Bunge. Kwanza kabisa, utaratibu wa Jeshi la Polisi kupiga marufuku maandamano ulikuwa ni ukiukaji wa sheria husika za nchi yetu.Mheshimiwa Spika,Kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi, mara baada ya taarifa ya maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA kutolewa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya, njia pekee halali ya kusitisha maandamano na mkutano uliopangwa ilikuwa ni kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha kutoa amri ya kusitisha maandamano na mkutano huo. Sheria hiyo inasema wazi kwamba Ofisa wa Polisi aliyepewa taarifa ya maandamano au mkutano wa hadhara hatatoa amri ya kuzuia au kusitisha maandamano au mkutano huo “isipokuwa tu kama amejiridhisha kwamba maandamano au mkutano huo unaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama na/au utulivu wa umma au kutumiwa kwa malengo haramu.”Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, chama cha siasa kikishatoa taarifa ya mkutano kinaruhusiwa kufanya mkutano huo isipokuwa tu na kama kitapokea amri kutoka kwa ofisa wa polisi mwenye mamlaka ya eneo husika ikielekeza kwamba mkutano huo usifanyike kama ilivyopangwa. Na chini ya sheria hii vile vile, ofisa wa polisi aliyepewa taarifa ya mkutano haruhusiwi kutoa amri ya kuzuia au kusitisha maandamano au mkutano huo mpaka atakapojiridhisha kwamba mkutano au maandamano hayo yana lengo la kutekeleza au kutumiwa kwa malengo haramu; au kama maandamano au mkutano huo unaweza au umelenga kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama na/au utulivu wa umma katika eneo husika.Mheshimiwa Spika,Kwa vyovyote vile, kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa, amri ya kuzuia na/au kusitisha maandamano au mkutano wa hadhara uliotolewa taarifa ni lazima itolewe na Mkuu wa Polisi wa Wilaya na ni lazima iwe ni ya maandishi. CHADEMA haijawahi kupokea wala kuonyeshwa amri ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha ya kupiga marufuku maandamano ambayo Mkuu huyo huyo wa Polisi wa Wilaya alikuwa ameyaruhusu kwa maandishi! Aidha, tumeona taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa na Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi tarehe 13 Januari 2011 ambayo imedai kwamba CHADEMA iliandikiwa barua yenye kumb. Na. ARR/B.5/1/VOL.VIII/24 ya tarehe 4 Januari 2011 iliyoandikwa na “Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa mujibu wa sheria … kusitisha maandamano hayo ya CHADEMA….” Madai hayo hayana ukweli wala msingi wowote kisheria kwa sababu Kamanda wa Polisi wa Mkoa hana mamlaka yoyote kisheria ya kusitisha au kupiga marufuku maandamano au mikutano ya hadhara. Mtu pekee mwenye mamlaka hayo chini ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa ni ‘ofisa polisi mwenye mamlaka ya eneo’ la mkutano, kwa maana nyingine, Mkuu wa Polisi wa Wilaya!Aidha, tuna taarifa kwamba jioni ya tarehe 4 Januari 2011 Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema alitangaza kwenye vyombo vya habari kwamba maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA yamepigwa marufuku kutokana na kuwepo kwa ‘taarifa za kiintelijensia’ kwamba kutakuwa na uvunjifu wa amani wakati wa maandamano na/au mkutano huo wa hadhara. Tangazo hilo la Inspekta Jenerali wa Polisi lilikuwa haramu na ni ukiukaji wa makusudi wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa kwa sababu Inspekta Jenerali wa Polisi hana mamlaka yoyote kisheria ya kuzuia au kuruhusu maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Vile vile utaratibu wa kutoa amri za kuzuia ama kusitisha maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa kutumia matangazo ya televisheni na/au waandishi wa habari ni utaratibu mgeni katika nchi ya Tanzania na hautambuliwi kabisa na sheria hizo!Mheshimiwa Spika,Hata kama ‘taarifa za kiintelijensia’ alizozisema Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema zilikuwa na ukweli - kwamba kulikuwa na uwezekano wa uvunjifu wa amani iwapo maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA ungeendelea kama ilivyokuwa imepangwa - bado Jeshi la Polisi la Tanzania lisingepaswa kutoa amri ya kuzuia na/au kusitisha maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA. Hii ni kwa sababu, kuzuia na/au kusitisha maandamano sio hatua pekee inayoweza kuchukuliwa kisheria na Jeshi la Polisi la Tanzania. Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, kila chama ambacho kimesajiliwa ‘kina haki ya kupatiwa ulinzi na msaada wa vyombo vya ulinzi kwa malengo ya kuwezesha mikutano yenye amani na utulivu.’ Swali la kumuuliza Waziri Mkuu hapa ni kwamba kama kweli kulikuwa na ‘taarifa za kiintelijensia’ za uwezekano wa uvunjifu wa amani, kwa nini Jeshi la Polisi lililokuwa na taarifa hizo halikutoa ulinzi wa kutosha kwa waandamanaji?Mheshimiwa Spika,Hata kama maandamano na mkutano wetu wa hadhara yangekuwa yamepigwa marufuku kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa – kitu ambacho hakikufanyika – bado CHADEMA ilikuwa na uhalali wa kuendelea na maandamano hayo na kufanya mkutano kama ilivyopangwa. Hii ni kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kulinda uhuru wa wananchi ‘kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani….’ Aidha, kwa mujibu ibara ya 64(5) ya Katiba, “… Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka mashrti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba, itakuwa batili.” Hii ina maana kwamba hata kama Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa inaruhusu Jeshi la Polisi kukataza na/au kusitisha maandamano, Sheria hizo zitakuwa ni batili kwa kiasi cha ukiukwaji wao wa masharti ya ibara ya 20(1) ya Katiba inayotoa uhuru wa kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara.4. UONGO WA NNE

Mheshimiwa Spika,Uongo wa nne aliousema Waziri Mkuu unahusu sababu ya kusitishwa kwa maandamano ya amani ya tarehe 5 Januari 2011. Kwa mujibu wa Hansard, Waziri Mkuu alitamka: “Sasa mkaamua kufanya maandamano yale bila kujali kabisa kwamba utaratibu uliokuwa wamekubaliana mmeukiuka wenyewe. Mheshimiwa Spika, sasa kilichotokea pale ni namna ya kuzuia hayo maandamano....” Kauli hii ya Waziri Mkuu ni ya uongo kwa sababu inapingana moja kwa moja na taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi iliyotolewa na Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi tarehe 13 Januari 2011.Kwa mujibu wa taarifa hiyo, “Jeshi la Polisi lilichukua hatua ya kuwaamuru waandamanaji kusitisha maandamano hayo mara moja baada ya kuona kwamba yataleta uvunjifu wa amani kutokana na jazba ya waandamanaji hao.” Wakati Waziri Mkuu – ambaye hakuwepo Arusha - anadai Bungeni kwamba maandamano yalisitishwa kwa sababu yalikiuka utaratibu, Jeshi la Polisi – lililokuwa na mamia ya askari polisi kwenye eneo la tukio – linasema kwenye taarifa rasmi kwamba maandamano hayo yalisitishwa kwa sababu ya jazba ya waandamanaji!. Taarifa ya IGP kama kielelezo “D”5. UONGO WA TANO

Mheshimiwa Spika,Uongo wa tano wa Waziri Mkuu unahusu kauli yake juu ya umbali kati ya Kituo Kikuu cha Polisi cha Arusha na mahali walipouawa waandamanaji watatu na wengine wengi kujeruhiwa. Kwa mujibu wa Hansard, Waziri Mkuu alitamka yafuatayo kuhusu jambo hili: “Mpaka mmekaribia mita 50 muweze kuingia kituo cha Polisi. Police was left with no option kwa kujua tu kwamba kama mkiingia hatujui litakalotokea ni kitu gani. Katika purukushani ile, masikini wale marehemu wale watatu wakapoteza maisha.”Kwa mara nyingine tena kauli ya Waziri Mkuu Bungeni inapingana na kauli ya Jeshi la Polisi. Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Jeshi hilo, “walipokaribia kituo Kikuu cha Polisi cha Kati umbali wa kama mita 50 huku wakirusha mawe, chupa, fimbo, nondo, mapanga na visu, amri halali na tahadhari za msingi zilizotolewa kuwataka watawanyike mara moja. Wafuasi hao walikaidi amri na kuzidi kukaribia kituo kwa lengo la kutimiza azma yao ya kukivamia.” Hapa maana ni kwamba waandamanaji walishapita huo umbali wa mita 50! Baada ya hapo, kufuatana na taarifa ya Jeshi la Polisi, hatua zifuatazo zilichukuliwa:

(i) Hatua ya kwanza, yalipigwa mabomu ya machozi, onyo ambalo lilipuuzwa na wakaendelea kusonga mbele;

(ii) Hatua ya pili, zilitumika risasi za baridi na mabomu ya vishindo bado walikaidi na kuzidi kukaribia kituo cha Polisi;

(iii) Hatua ya tatu, zilipigwa risasi juu za onyo bado wakaendelea kusonga mbele.

Mheshimiwa Spika,Baada ya hatua zote hizo kushindikana kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, “kilichofuatia ni mapambano ya ana kwa ana kati ya askari na waandamanaji waliokuwa wakisonga mbele kuvamia kituo. Katika mazingira hayo risasi za moto ililazimika kutumika. Matokeo ya tafrani hiyo, watu 14 walijeruhiwa na kufikishwa hospitalini ambapo watatu kati yao walifariki dunia wakipatiwa matibabu.”Mheshimiwa Spika,Kama ni kweli hatua zote zilizoelezwa hapo juu zilichukuliwa na Jeshi la Polisi basi ni wazi kwamba watu waliouawa au kujeruhiwa waliuawa au kujeruhiwa kwenye uzio au mlango wa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Arusha! Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwa kauli ya Waziri Mkuu, taarifa ya Jeshi la Polisi vile vile ni ya uongo mtupu. Kwa ushahidi wa picha za video tulio nao, marehemu mmoja aliuawa kwenye eneo la Mianzini ambalo liko zaidi ya kilometa tatu kutoka Kituo Kikuu cha Polisi cha Arusha. Aidha, marehemu wa pili alipigiwa risasi katika eneo la Kaloleni ambalo nalo liko zaidi ya kilometa moja kutoka kituo hicho. Ushahidi wa video unaungwa mkono na ushahidi wa watu walioshuhudia mauaji hayo wenyewe.6. UONGO WA SITA

Mheshimiwa Spika,Uongo wa sita wa Waziri Mkuu unatokana na kauli yake kwamba “... kama Mheshimiwa Mbowe na chama chako mngeliamua kushirikiana na Serikali hii mkafanya ule mkutano kama tulivyokubaliana haya yote yasingetokea.” Ukweli ni kwamba mkutano wenyewe uliohutubiwa na Dr. Wilbrod Slaa na Mheshimiwa Philemon Ndesamburo ulishambuliwa kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwashawasha na kutawanywa kabla ya makundi ya watu kurudi kwenye mkutano na Dr. Slaa na Mheshimiwa Ndesamburo kuendelea kuhutubia!Aidha, ushahidi wa maandishi kati ya CHADEMA na Jeshi la Polisi Wilaya ya Arusha unaonyesha wazi kwamba CHADEMA walikubaliana na matakwa ya Jeshi la Polisi kwa kuchagua njia moja ya maandamano. Hata viongozi waliokamatwa wakati wa maandamano hayo walikamatiwa kati ya eneo la Sanawari na Mianzini wakiandamana kwa kutumia moja ya njia zilizopendekezwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya! Na gari iliyokuwa imewabeba Mheshimiwa Lucy Owenya na mke wa Dr. Slaa ilishambuliwa na kuvunjwa vioo na Mheshimiwa Owenya na Mama Slaa kuumizwa na askari polisi katika eneo la Sanawari Mataa wakati wakiwa katika njia ya maandamano iliyopendekezwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba, waliovunja makubaliano juu ya maandamano na mkutano wa hadhara walikuwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa ACP Thobias Andengenye na Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema walioamua kuingilia maamuzi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha na kuyapiga marufuku maandamano hayo.7. UONGO WA SABA

Mheshimiwa Spika,Katika jibu lake kwa swali la Mheshimiwa Martha Umbulla, Waziri Mkuu alidai kwamba mkutano wa Baraza la Madiwani wa kumchagua Meya, Naibu Meya na Wenyeviti wa Kamati ulianza “wajumbe wote 31 wakiwepo....” Hii ni kauli ya uongo. Kwa mujibu wa kanuni ya 11 ya Kanuni za Kudumu za Mikutano na Shughuli za Halmashauri ya Manispaa ya Arusha za 2003, “kila mjumbe anayehudhuria mkutano wa Halmashauri au Kamati yoyote ya Halmashauri ambamo yeye ni mjumbe ataweka sahihi yake kwenye Rejesta ya mahudhurio inayotunzwa na Mkurugenzi kwa ajili hiyo.” Kwa kufuatana na orodha ya mahudhurio ya mkutano wa tarehe 17 Desemba, walikuwepo madiwani 16 wote wakiwa madiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM)!Kwa Waziri Mkuu kusimama na kuliambia Bunge kwamba wajumbe wote 31 wa Halmashauri ya Jiji la Arusha walikuwepo tarehe 17 Desemba 2010 wakati Rejesta ya mahudhurio inaonyesha kwamba ni wajumbe 16 tu ndio walioweka sahihi zao kwenye Rejesta hiyo ni uongo wa wazi. Angalia Kielelezo “E”Mheshimiwa Spika,Waziri Mkuu alitoa kauli ya uongo tena pale aliposema kwamba mgombea wa CCM alishinda kura za meya “walikuwa wanashindana mmoja wa CHADEMA, mmoja wa CCM.” Kwa mujibu wa orodha ya mahudhurio ya mkutano wa tarehe 18 Desemba 2010 uliomchagua Meya, waliokuwepo ni madiwani 17 ambao kati yao, 16 walikuwa wa CCM na mmoja alitoka chama cha TLP. Hakukuwepo na mjumbe hata mmoja wa CHADEMA. Na hii haishangazi kwa sababu ratiba ya mkutano huo inaonyesha kwamba siku ya tarehe 18 Desemba 2010 ilitakiwa kuwa siku ya mafunzo ya Madiwani yaliyokuwa yafanyike Olasiti Garden. Madiwani wa CHADEMA ambao hawakuwepo kwenye mkutano wa tarehe 17 Desemba wasingeweza kujua kwamba ratiba ya mafunzo ilikuwa imebadilishwa na kuwa ratiba ya uchaguzi wa Meya! Ratiba ya shughuli za tarehe 18.12.2010 kielelezo “F”8. UONGO WA NANE

Mheshimiwa Spika,Uongo wa nane wa Waziri Mkuu ni kauli yake kwamba “... utaratibu uliofuatwa ulikuwa sahihi kabisa, haukukosewa kitu chochote. Meya ni halali kabisa, alipatikana kihalali kabisa.” Huu ni uongo mtupu. Chini ya kanuni ya 8(3) ya Kanuni za Halmashauri, “akidi katika mkutano wa kawaida wa mwaka na mkutano wa kwanza wa Halmashauri itakuwa theluthi mbili ya wajumbe wote wa Halmashauri.” Kwa kusoma kanuni ya 8(3) pamoja na kanuni ya 9, ni wazi kwamba Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri wanatakiwa kuchaguliwa na mkutano wa kwanza wa Halmashauri. Ili kukidhi matakwa ya kanuni hizi, mkutano wa uchaguzi wa Meya na Makamu Meya wa Arusha ulipaswa kuwa si chini ya wajumbe 21 ambao ni theluthi mbili ya wajumbe wote wa Halmashauri hiyo. Kwa maana hiyo, mkutano wa tarehe 18 Desemba haukuwa mkutano halali na viongozi wa Halmashauri waliochaguliwa na mkutano huo hawawezi kuwa halali!9. UONGO WA TISA

Mheshimiwa Spika,Uongo wa tisa aliousema Waziri Mkuu Bungeni uko kwenye kauli ifuatayo: “Mheshimiwa Spika, yaani hata kwa hesabu tu za kawaida za mtoto wa darasa la kwanza hakuna namna ambavyo kwa hali ilivyokuwa kwamba mna CHADEMA wajumbe 14, una CCM 16 utashindaje?” Hapa Waziri Mkuu alitaka kuaminisha Bunge kwamba hata kama wajumbe wa CHADEMA wangehudhuria kwenye mkutano huo bado wasingeshinda kwa sababu wajumbe wa CCM walikuwa wengi zaidi ya wajumbe wa CHADEMA. Lakini kwenye hotuba hiyo hiyo Waziri Mkuu alitoa kauli ifuatayo kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Naibu Meya wa Halmashauri hiyo ya Arusha: “Wakaingia awamu ya pili ya kumtafuta Naibu Meya, wakapiga kura, Mjumbe wa kutoka TLP akashinda, CCM alishindwa hakupata kura hata moja, CHADEMA hawakupata kura hata moja...”!Mheshimiwa Spika,Kwa akili za kawaida za mtoto wa darasa la kwanza kama iliwezekana kwa mgombea wa TLP ambaye yuko peke yake katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kupata kura za wajumbe wote wa CCM na kumshinda mgombea wa CCM ambaye – kwa kauli ya Waziri Mkuu – hakupata kura hata moja, je, ingeshindikanaje kwa mgombea wa CHADEMA yenye wajumbe 14 kushinda? Swali ni muhimu hasa hasa kwa vile chini ya kanuni ya 9(1) ya Kanuni za Kudumu za Halmashauri ya Jiji la Arusha inasema kwamba kura ya kumchagua Mwenyekiti na Makamu wake itakuwa ni ya siri! Na kama inavyofahamika, katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, ni mgombea wa CHADEMA ndiye aliyeshinda pamoja na kwamba CCM ina wajumbe wengi zaidi katika Halmashauri hiyo!10. UONGO WA KUMI

Mheshimiwa Spika,Waziri Mkuu aliulizwa swali la nyongeza na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kama Serikali iko tayari kuunda tume ya uchunguzi ya kimahakama kutafuta ukweli wa matukio ya Arusha na “... vile vile kuchukua hatua kwa wale wanaohusika.” Swali hilo liliulizwa pia na Mheshimiwa Martha J. Umbulla aliyetaka kujua kama Serikali itachukua hatua kuwaadhibu CHADEMA kwa kile alichokiita kuhusika na vurugu za Arusha “... ili tukio kama hilo lisirudie katika chaguzi za nchi yetu?” Waziri Mkuu alijibu: “Mimi nadhani hili ... wala si suala pengine la kusema ichukue hatua dhidi ya CHADEMA hapana.” Waziri Mkuu alitilia mkazo kwamba Serikali haina mpango wa kuwachukulia hatua CHADEMA kwa kusema: “Nataka niwaombe sana, hili hatuwezi kama Serikali tukasema tutaichukulia hatua CHADEMA....”. Angalia hansard ya tarehe 10-02-2011 kielelezo “G”Mheshimiwa Spika,Watanzania wawili na raia wa nchi jirani na yenye uhusiano mzuri na nchi yetu waliuawa wakati wa vurugu za Arusha. Watu wengine wengi walijeruhiwa kwa kupigwa risasi, mabomu, virungu na mabuti ya polisi. Kama taarifa za Jeshi la Polisi na kauli ya Waziri Mkuu ni za kweli, vurugu hizo zilihusisha pia mashambulizi na uharibifu wa mali za Serikali kama vile vituo vya Polisi na mali za watu binafsi na za vyama vya siasa hususan CCM. Aidha, kama kauli ya Jeshi la Polisi nay a Waziri Mkuu ni za kuaminiwa, madhara yote haya yalitokana na uchochezi uliofanywa na viongozi wa ngazi za juu wa CHADEMA na ambao wametajwa kwa majina.Mheshimiwa Spika,Kama yote haya ni ya kweli na sio porojo za kisiasa, Watanzania wanapaswa kuambiwa ni kwa nini Serikali hii haiko tayari kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliohusika na matukio haya? Kwa nini Serikali imeamua kwamba ni busara kuwafungulia mashtaka ya kosa dogo la kufanya maandamano kinyume cha sheria badala ya kuwashtaki kwa makosa makubwa kama kusababisha mauaji, au uchochezi, au kujaribu kuchoma majengo moto au makosa ya aina hiyo ambayo yana adhabu kubwa zaidi ya kosa waliloshtakiwa nalo? Kukataa kuchukua hatua stahili kuna tafsiri moja tu: CHADEMA hawakuhusika katika vurugu za Arusha na kwa hiyo kauli ya Waziri Mkuu Bungeni ni ya uongo na yenye lengo la kulidanganya Bunge!HITIMISHO

Mheshimiwa Spika,Kanuni ya 63(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007, inasema “… ni marufuku kabisa kusema uongo Bungeni na kwa sababu hiyo, Mbunge yeyote anapokuwa akisema Bungeni ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anatoa kauli au maelezo kuhusu jambo au suala ambalo yeye mwenyewe anaamini kuwa ni la kweli na siyo jambo la kubuni au la kubahatisha tu.” Hii pia ni msingi wa kanuni ya 64(1)(a) ya Kanuni za Bunge.Kama nilivyothibitisha katika maelezo haya, Waziri Mkuu amesema uongo na/au kutoa taarifa ambazo hazina ukweli Bungeni. Kanuni ya 63(5) inaelekeza cha kufanya inapothibitika kuwa Mbunge amesema uongo Bungeni: “Spika au Mbunge mwingine yeyote, baada ya kutoa maelezo mafupi ya ushahidi unaotilia mashaka ya dhahiri kuhusu ukweli wa kauli au usemi au maelezo juu ya jambo au suala ambalo Mbunge amelisema Bungeni, anaweza kumdai Mbunge huyo atoe uthibitisho wa ukweli wa kauli au usemi au maelezo yake na kama atashindwa kufanya hivyo, afute kauli au usemi au maelezo yake hayo.” Naomba kuchukua nafasi hii kumtaka Waziri Mkuu atoe uthibitisho wa ukweli wa kauli au usemi au maelezo yake Bungeni siku ya tarehe 10 Februari 2011 na kama atashindwa kufanya hivyo, afute kauli au usemi au maelezo yake hayo na kutubu kwa Mungu!Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha!

Godbless Jonathan LemaMbunge wa jimbo la Arusha Mjini

ramani ya tovuti kanusho la hatia © 2011 chadema.or.tz tuandikie mtunza tovuti

Imesasaishwa 2011-02-18 Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli juu

No comments: