Pages

Saturday, April 30, 2011

WHO watua Samunge

Saturday, 30 April 2011 08:54

0diggs

digg

Wanasayansi wa ndani wathibitisha uwezo wake

Mussa Juma, Samunge

WATAALAMU wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na taasisi mbalimbali za afya nchini, jana walifika Samunge kuanza mchakato wa kutafiti dawa inayotolewa na Mchungaji, Ambilikile Mwasapila kama inatibu magonjwa sugu au la.Wataalamu hao walifika Samunge majira ya saa sita mchana na kusababisha kusitishwa kwa muda utoaji wa tiba ili kuwapa nafasi ya kufanya mahojiano na Mchungaji Mwasapila, kuchukua sampuli za dawa na mti ya mugariga. Baada ya mahiojiano, nao pia walipata kikombe cha tiba.Wataalamu hao ni pamoja na Profesa Charles Wambebe wa WHO Marekani, Dk Budeba Sylvester wa Wizara ya Afya na Dk Georges Shemdowe kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia.Ujumbe wa huo pia ulimjumuisha, Mkemia kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Hamis Malebo.Profesa Wambebe ambaye ni raia wa Nigeria na mtaalamu bingwa mwenye uzoefu na masuala ya tiba za asili, alisema amefika Samunge kutokana na maombi ya Serikali ya Tanzania iliyoomba msaada wa WHO, kufanya uchunguzi wa dawa ya Mchungaji Mwasapila.''Tumekuja hapa Samunge, kufuatilia tiba hii jinsi inavyotolewa na WHO kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania itaendesha utafiti kwa kuhusisha watu waliotumia dawa, Mchungaji Mwasapila na wadau wengine ili kuona inaponyesha kiasi gani," alisema Profesa Wambebe.Alisema wanatarajia kuwa ndani ya miezi 12 watakuwa wametoa majibu juu ya ubora wa dawa hiyo na katika kipindi cha miezi mitatu ijayo watatoa maendeleo ya utafiti ambao utakuwa unafanywa.Alisema baada ya kukamilisha utafiti, Serikali ya Tanzania ndiyo itakayoachiwa jukumu la kutangaza dawa hiyo kama inatibu kiasi gani na kama itahitaji kuboreshwa ili iwe katika mazingira ya kisasa ni nini kifanyike.Wagonjwa wa kisukari kuanza

Dk Sylvester alisema uchunguzi huo utaanzia kwa wagonjwa wa kisukari hasa kutokana na vipimo vyao kuwa rahisi na kufuatilia hali zao pia itakuwa ni rahisi tofauti na magonjwa mengine.Alisema wizara ya afya inakusudia kupeleka Samunge, maabara kubwa ya kisasa ambayo wagonjwa watapimwa kabla ya kunywa dawa na baada ya kunywa watafuatiliwa kitaalamu hadi hapo itakapothibitika ubora wa dawa."Tunaomba wananchi wasubiri watafiti kufanya kazi kwani tayari taarifa ilitolewa kuwa dawa hii haina madhara kwa binadamu na kazi inayofuatia sasa ni kutazama ubora wake katika kutibu maradhi mbalimbali," alisema.

Babu atoa shukraniKatika hatua nyingine, Mchungaji Mwasapila jana alitoa shukrani kwa serikali kuanzia ngazi ya Kijiji hadi wilaya kutokana ushirikiano waliompa katika msiba wa mtoto wake, Jackson (43) ambaye alifariki wilayani Babati baada ya kuugua malaria."Napenda kushukuru Serikali Wilaya ya Ngorongoro na Babati kwa msaada mkubwa ambao wamenipa katika msiba na kuniwezesha kufika kwa wakati na kurejea hapa, pia nawashukuru wananchi wote kwa ushirikiano walionipa," alisema Mwasapila.Uchunguzi wa NIMRI,MUHASNaye Leon Bahati anaripoti kuwa,Uchunguzi wa awali uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Muhimbili (MUHAS) umebaini kwamba dawa ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapila ina uwezo wa kutibu magonja sugu zaidi ya sita.Katika ripoti yao wamependekeza kufanyika kwa utafiti zaidi juu ya uwezo wa dawa hiyo katika tiba, usalama, kiwango cha dozi anachopaswa kutumia mgonjwa na muda wa matumizi.Wataalamu waliochunguza dawa hiyo iliyosisimua na kuvuta watu wengi ndani na nje ya nchi kwenda katika Kijiji cha Samunge, Wilaya ya Loliondo, Arusha kwenda kupata dawa hiyo wamesema imewastaajabisha kwa namna ilivyo na kemikali nyingi zenye uwezo wa kuimarisha afya ya binadamu.Wataalamu hao, Profesa Hamisi Malebo na Profesa Zakaria Mbwambo wamesema utafiti huo wa awali umeonyesha kuwa dawa hiyo ina uwezo wa kudhibiti ugonjwa wa kisukari, moyo, saratani, ini, malaria, Ukimwi na magonjwa mengine yanayosababisha uvimbe mwilini, vidonda pamoja na athari za bakteria mwilini.Magonjwa mengine yanatajwa kuwa ni ya mfumo wa chakula, athari za mfumo wa akili na moyo kushindwa kufanya kazi sawasawa.“Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapaswa kuendesha majaribio ya utafiti ili kujibu maswali muhimu kama vile usalama wa dawa hiyo katika mwili wa binadamu, dozi yake pamoja na muda wa matumizi kulingana na aina ya ugonjwa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo yenye kurasa 25.Jambo jingine ambalo wataalamu hao kutoka katika vitengo vya tafiti za dawa za asili wa NIMR na MUHAS, wanalisisitiza katika utafiti huo ni uwiano wa kemikali kwenye dawa ya mti huo walioupa jina kuwa ni wa maajabu.Ripoti hiyo ambayo Mwananchi ilifanikiwa kuiona, ina sehemu saba ambazo zinajumuisha shukurani kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kugharimia utafiti huo, maelezo kuhusu mti huo wa ajabu, muoanisho wa mti huo kibaiolojia, njia walizotumia kutafiti na matokeo yake, maelezo ya majumuisho na mapendekezo.Uchunguzi wa kimaabara

Ripoti hiyo inaeleza kwamba katika kuchunguza sumu iliyopo katika mti huo, walitumia panya na kubaini kwamba ni salama pale ambako haitumiki mizizi hiyo moja kwa moja.Wataalamu hao wanaeleza njia anayotumia Mchungaji Mwasapila ya kuichemsha na kutoa dozi ya milimita 200 kwa mgonjwa ni salama na haiwezi kumuathiri binadamu kiafya.Wanasema kemikali zilizopo kwenye mti huo zimeonekana kuwa na uwezo wa kudhibiti magonjwa kama ambavyo Mchungaji Mwasapila amekuwa akieleza.Wanasema walipompa panya dawa hiyo, iliweza kuweka uwiano mzuri wa sukari kwenye mfumo wa damu hivyo kuashiria kwamba ina uwezo wa kutibu kisukari.Hali hiyo inaelezwa kuwa inatokana na mti huo kuwa na mfumo unaoweza kusababisha muanisho wa utoaji wa insulini ambayo kwenye mwili wa binadamu ni muhimu katika kusawazisha kiwango cha sukari mwilini.Kuhusu ugonjwa wa moyo, wataalamu hao wanasema dawa ya Babu ina uwezo wa kushusha mapigo ya moyo ambayo yako juu hivyo kuweza kudhibiti maradhi hayo.Mti huo pia umeonekana kuwa na uwezo wa kurekebisha ini ambalo halifanyi kazi zake inavyotakiwa hivyo kutibu aina zote za magonjwa zinazotokana na athari za kushindwa kwake kufanya kazi.Kwa mujibu wa maelezo ya kitaalamu, moja ya kazi za ini ni kuondoa sumu mwilini na iwapo halifanyi kazi zake sawasawa, sumu hizo husababisha madhara mbalimbali kwenye mwili wa binadamu.Wameuelezea uwezo huo kuwa unasaidia kupambana na ugonjwa sugu wa saratani.Utafiti huo pia umeonyesha kuwa mti huo wa maajabu una uwezo wa kudhibiti virusi wa aina mbalimbali kama vile vya Ukimwi na polio. Wataalamu hao walieleza kwamba walipojaribu kulinganisha panya walioambukiza virusi, aliyetibiwa kwa mti huo aliongeza uwezo wa kuendelea kuishi kwa kati ya asilimia 28 hadi 35 ukilinganisha na yule ambaye hakutibiwa.Ilionekana pia kuwa panya walioathiriwa na virusi waliotibiwa na dawa hiyo waliepushwa na uwezekano wa vitoto vyao vilivyozaliwa kufa mapema kwa asilimia 70 hadi 90.Kwa sababu hiyo, wanasayansi hao wakahitimisha kwamba maelezo ya Mchungaji Mwasapila kuhusu tiba ya Ukimwi ina ukweli ndani yake.Kemikali za mti wa maajabuBaada ya kuchunguza mti huo wa maajabu kimaabara, wataalamu hao walibaini kwamba una kemikali nane muhimu.Kemikali hizo zinajulikana kwa majina ya kitaalamu; steroids, terpenes, benzenoids, phenylpropanoid, lignans, coumarins tannins, flavonoids na cardiac glycosides.

Sesquiterpenes (trpenes) ni kemikali ambayo kitaalamu inajulikana kuwa ina uwezo wa kukabili bakteria, malaria, saratani na visababishio vya uvimbe mwilini.Triterpenes inajulikana kitaalamu kuwa inatibu athari mbalimbali za mifumo ya mwili kama vile njia ya mkojo na uvimbe mwilini.Kemikali nyingine pia zinasaidia kuweka usawa lehemu (cholesterol) kwenye mfumo wa damu na nyingine kama vile ‘ursolic acid’ hupunguza nguvu ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kuzaliana kwenye mwili wa binadamu.Kemikali nyingine phenylpropanoids na phenylethanoids zipo kwenye kundi la pili la kemikali zinazopatikana kwenye mimea ambazo kazi yake kubwa ni kutibu vidonda, athari za hewa chafu na mazingira ya hewa yenye athari za mwili.Coumarins husaidia mambo mbalimbali mwilini athari za moyo hasa zinazosababisha kupungua uwezo wa kusukuma damu na kutibu athari za mfumo wa chakula pamoja na wa akili.Historia ya mti wa maajabuMambo yasiyo ya kawaida kuhusu mti huo wa ajabu yanaelezwa kwamba yalijitokeza kwa kasi katika Kijiji cha Samunge Agosti, 2010.“Watu wengi walifurika katika Kijiji cha Samunge kutoka sehemu mbalimbali nchini kwa lengo la kupata tiba ya magonjwa sugu,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.Wametaja magonjwa hayo sugu kuwa ni kisukari, Ukimwi, pumu, saratani na kupooza ambayo wanaeleza kuwa Mchungaji Mwasapila alikiri anayatibu baada ya kuoteshwa tangu mwaka 1991.Katika uchunguzi wao, wataalamu hao walisema mti huo una majina mbalimbali kutokana na makabila tofauti mkoani Arusha.Wanasema Mchungaji Mwasupila aliwaambia mti huo unaitwa “mugariga” wakati Wamasai wanauita “engamuriaki” au “olmuriaki” na kabila la Wasonjo linauita “engamuriaga.”Kulingana na maelezo waliyoyapata kutoka kwa mchungaji huyo, wakati wa maandalizi ya dawa hiyo, huchemsha mizizi yake kwa saa moja na baadaye huachwa ipoe kabla ya matumizi.Jambo ambalo liliwashangaza wataalamu hao ni kwamba mchungaji huyo maarufu kwa jina la Babu, amekuwa akisisitiza kwamba ili dawa hiyo ifanye kazi ni lazima yeye binafsi aimimine kwenye kikombe atakachokunywa mgonjwa. Kikombe chake huwa anakitumia kama kipimo.Uchambuzi wa mti kisayansiWataalamu hao walisema baada ya kuuchunguza mti huo walibaini kitaalamu unaitwa carissa spinarum ambao upo katika jamii ya apocynaceae.Wanauelezea kuwa ni mti wenye miiba na utomvu kama maziwa, majani yenye kijani cha kukolea kwa juu na chini yake viotea kama nywele laini na mti humea hadi urefu wa mita tano kutoka usawa wa ardhi.Katika kuzaa, wanasema mti huo hutoa maua meupe na mchanganyiko wa rangi nyingine kama vile nyekundu, pinki na zambarau.“Huzaa matunda ya mviringo yenye kipenyo kinachokadiriwa kuwa sentimita 1.1 na yanapoiva huelekea kuwa na rangi nyeusi… Ukiyala ni matamu na ya kufurahisha. Ndani huwa na mbegu mbili hadi nne,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.Nchi ambazo mti huo unaweza kupatikana zinatajwa kuwa ni Australia, Botswana, Cambodia, Cameroon, Eritrea, Ethiopia, Ghana, Guinea, Japan, Kenya, Myanmar, Namibia, Nigeria, Papua, Saudi Arabia, Senegal, Afrika Kusini, Sudan, Thailand, Uganda, Vietnam na Yemen.Matumizi ya mti huo kijadi

Wamasai wanaelezewa kuwa wamekuwa wakiutumia mti huo kama sehemu ya kunogesha chakula. Jamii nyingine za hapa nchini zinazoutumia ni Wasonjo, Wagogo, Wakurya na Wabarbaig.Uchunguzi wa pia umebaini kwamba Ghana hutumia matunda ya mti huo pamoja na chakula kama sehemu ya kumfanya mgonjwa kupata hamu ya kula.Katika nchi nyingine kama Kenya na Sudani, hukamua mbegu zake ili kupata juisi.Katika bara la asia baadhi ya watu wanaelezewa kuwa huitumia mizizi yake kwa ajili ya kuzuia kuharisha.Pamoja na maelezo mazuri ya utafiti huo wa awali, wataalamu hao wamesema serikali inapaswa kuweka mkakati wa utafiti wa kina zaidi ili kuwa na mkakakti bora wa kitaalamu kuhusu dawa hiyo.Miongoni mwa mapendekezo yao ni kuitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutoa fedha kwa ajili ya utafiti huo ambao utatoa picha halisi ya tiba za mti huo wa ajabu na hasa kujibu maswali muhimu ya uwezo wake katika tiba, usalama, kiwango cha dozi anachopaswa kutumia mgonjwa na muda wa matumizi.

No comments: