Urais wa Kikwete utata mtupu
--------------------------------------------------------------------------------
Na Saed Kubenea - Imechapwa 15 December 2010
MATOKEO ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa Oktoba mwaka huu, yanazidi kuzua utata, MwanaHALISI limeelezwa.
Kungundulika kwa utata zaidi wa matokeo hayo kumefuatia kukamilika kwa kazi ya kukusanya, kuhesabu na kuhakiki matokeo ya uchaguzi iliyofanywa kwa ustadi mkubwa na viongozi wa ngazi ya juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
CHADEMA ilituma maofisa wake kukutana na mawakala wake kwenye vituo na kwenye ngazi ya jimbo kwa shabaha ya kutaka kujua usahihi wa kura ambazo chama hicho kilipata.
Taarifa za ndani ya chama hicho zinasema, maofisa walitumwa katika mikoa 24 ya Tanzania Bara na Visiwani kufanya kazi ya kukusanya matokeo.
Tayari ripoti ya matokeo hayo imewasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu (CC) kilichofanyika Jumamosi iliyopita, jijini Dar es Salaam.
Inaelezwa kuwa matokeo hayo yanapishana kwa kiasi kikubwa na matokeo ambayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza.
Kwa mfano, matokeo katika jimbo la Ilala, mkoni Dar es Salaam, NEC ilitangaza kuwa mgombea urais wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa amepata kura 18,513, huku rais Kikwete akipata kura 35,910.
Lakini matokeo ambayo yamekusanywa na CHADEMA, kutoka mawakala wake, yanaonyesha kuwa katika jimbo hilo, rais Kikwete alipata kura 20,120, huku Dk. Slaa akipata kura 26,724.
Kuendelea kuibuka kwa utata kunakuja wiki sita baada ya NEC kumtangaza mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete kuwa mshindi wa kiti hicho.
Katika uchaguzi huo, NEC ilimtangaza Dk. Willibrod Slaa, ambaye aligombea urais kupitia CHADEMA, kushika nafasi ya pili.
Katika jimbo la Vunjo, NEC ilimtangaza Kikwete kupata kura 27,649 huku Dk. Slaa akitangazwa kupata kura 22,442.
Lakini matokeo yaliyokusanywa na CHADEMA yanaonyesha kuwa Kikwete amepata kura 24,574 huku Dk. Slaa akipata kura 20,841. Katila jimbo la Geita, mkoani Mwanza, NEC ilitangaza kuwa rais Kikwete amepata kura 17,792 huku Dk. Slaa akiambulia kura 3,789.
Bali matokeo yaliyokusanywa na CHADEMA katika jimbo hilo, kwa mujibu wa nyaraka zilizokusanywa, yanaonyesha kuwa Rais Kikwete amepata kura 30,950, huku Dk. Slaa akiwa amepata kura 15,796.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya kikao cha CC, wajumbe kwa kauli moja, walikubaliana kuwa kwa ushahidi uliokusanywa, kura zilizotangazwa na NEC hazikuwa zenyewe na matokeo hayakuwa sahihi wala halali.
“Baada ya yote hayo, wajumbe wamekubaliana kwa kauli moja, kwamba kura zilizotangazwa na NEC, si halali. Kilichotangazwa na NEC si matokeo halisi ya uchaguzi,” ameeleza mmoja wa viongozi wa chama hicho.
MwanaHALISI lilipomuuliza Dk. Slaa juu ya kuwapo kwa tofauti hiyo ya kura, haraka alisema, “Hatufanyi vitu kwa kubahatisha. Tulipowaambia kwamba matokeo yanayotangazwa na NEC ni ya kupikwa na usalama wa taifa, wengi hawakutuelewa.”
Alisema, “Tunajiandaa kuanika kila kitu hadharani. Tutazungumza na waandishi wa habari kama siyo kesho (jana), basi kesho kutwa (leo). Subiri, utapata kila kitu.” Alipotakiwa kueleza hatua zitakazochukuliwa na chama chake, baada ya kugundua kasoro hizo, Dk. Slaa alisema, “Hayo tutayaeleza baadaye.”
Alipong’ang’anizwa kusema ni hatua gani za haraka watachukua, alijibu kwa ufupi tu, “Tutapeleka kilio chetu kwa wananchi kwa njia ya amani.”
Akiongea kwa kujiamini, Dk. Slaa alisema, “Wewe unajua kuwa CHADEMA si chama cha vurugu. Hiki ni chama kinachoamini katika misingi ya amani na utulivu.”
Dk. Slaa amekuwa akisisitiza kwamba hayuko tayari kuingia ikulu wakati damu ya Watanzania inachuruzika. Alisema, “Tunataka kuhakikisha makosa haya hayarudiwi tena. Tunatambua serikali iliyopo hata kama haikuchaguliwa kwa njia ambazo ni mwafaka. Lakini kwa kuwa sheria zinazuia kupinga matokeo yaliyotangazwa, tutaendelea kulundika madai mengine ya msingi na kumtaka rais achukue hatua ya kuyatekeleza.” Mazungumzo kati ya Dk. Slaa na gazeti hili yalifanyika juzi Jumatatu.
Mtoa taarifa kwa gazeti hili amesema ushahidi ambao CHADEMA imeupata, ni pamoja na kile inachoita, “matokeo halisi ya uchaguzi” kutoka kituo hadi kituo.
Miongoni mwa matokeo ambayo yamekusanywa na ambayo yanatiliwa shaka, ni pamoja na matokeo ya urais katika jimbo la Kilombero, mkoani Morogoro na Mtoni, Zanzibar.
Katika jimbo la Kilombero, msimamizi wa uchaguzi, Pius G. Maffa alibatilisha matokeo saa chache baada ya kutangaza matokeo ya awali. Katika barua yake ya tarehe 4 Novemba 2010, yenye Kumb. Na. KDC/E30/8/VOL VI/155 yenye kichwa cha habari kisemacho, “…Majumuisho ya kura za urais,” Maffa anasema matokeo aliyotangaza awali hayakuwa halali.
Maffa katika barua yake hiyo aliyoituma kwa makatibu wa vyama vyote katika jimbo lake, anasisitiza “…pamoja na barua hii, naambatanisha fomu Na. 24A iliyojazwa upya kutokana na hitilafu za kiufundi zilizoonyeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.”
Hitilafu ambazo Maffa anadai zilionekana baada ya matokeo hayo kupelekwa NEC, ni sehemu ya malalamiko ya CHADEMA; hata pale ambapo matokeo hayo yanaonekana kubadilishwa, bado yanapingana na ukweli halisi.
Katika jimbo la Mtoni, katika kituo cha kupigia kura kilichopachikwa jina la Mtoni School, NEC iliorodhesha wapigakura 350 kwa kila kituo kidogo cha kupigia.. Katika kituo hicho Na. 00025763, na ambacho kilikuwa na vituo vidogo A,B,C,D,E, NEC ilidai kuwa kila kituo kilikuwa na wapigakura 350 na kwamba ni wapigakura 200 waliojitokeza katika kila kituo.
“Yaani wewe unaweza kuamini kuwa wapigakura walioandikishwa kupigakura kwa kila kituo katika vituo hivyo vidogo ni 350, huku waliojitokeza kupigakura walikuwa 250? Watu hao ndiyo waliojitokeza kwa kila kituo? Hii inaonyesha kwamba hawa watu walijifungia na kutunga hesabu zao,” anaeleza mtoa taarifa wetu.
Anasema, “Matokeo haya ya uchaguzi, tayari yametuathiri. Mbali na mapungufu ya uhalali wa kiti cha urais, yameathiri idadi ya wabunge wa viti maalum na ruzuku ambayo chama kingepata.”
CHADEMA imeorodhesha madai makuu ambayo wanataka serikali iwe imeanza kuyatekeleza ndani ya kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa. Madai hayo, kwa mujibu wa mtoa taarifa, ni pamoja na kuandikwa kwa katiba mpya; na kuundwa upya kwa tume ya taifa ya uchaguzi.
“Kwanza, tunataka serikali iandae mchakato wa kupatikana katiba mpya. Lengo ni kupatikana katiba mpya kabla ya uchaguzi mwaka 2015,” ameeleza mtoa taarifa.
Pili, “Tunataka serikali iunde upya tume ya ya taifa ya uchaguzi na tatu, serikali ikubali kuunda tume huru ya kuchunguza wizi na upotevu wa kura.”
Gazeti toleo na. 219
source:http://www.mwanahalisi.co.tz
No comments:
Post a Comment