Vigogo walikula rushwa ununuzi wa rada Send to a friend
Tuesday, 21 December 2010 21:21
0diggs
digg
Waandishi Wetu
KESI ya ufisadi katika ununuzi wa rada jana ilitolewa huku kwa kufunika suala la rushwa baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Southwark Crown ya jijini London, Uingereza kuipiga faini ya Pauni 500,000 za Kiingereza (sawa na Sh1.1 bilioni za Tanzania) kampuni ya BAE System kwa kushindwa kutunza taarifa za malipo ya mshauri wao wa kiufundi ambaye ni Mtanzania.
Hukumu hiyo imetolewa siku moja baada ya Jaji David Michael Bean kutilia shaka malipo ya dola 12.4 milioni kwa mfanyabiashara wa Kitanzania, Shailesh Vithlani ambaye alikuwa wakala wa BAE, akisema kuwa fedha hizo zilitumika kuwapa rushwa viongozi wa serikali ya Tanzania ili wakubali mpango huo wa kununua rada kwa bei ya juu.
Jaji Bean alitishia kutotoa hukumu inayoidhinisha makubaliano yanayoitaka BAE System ilipishwe faini hiyo, akitaka maelezo ya malipo hayo kwa kuwa alisema inaonekana kuwa Vithlani angeweza kutumia fedha hizo kumrubuni mtu yeyote ili mradi apewe zabuni hiyo ya kununua rada kwa dola 40 milioni za Kimarekani.
Lakini Jaji Bean alijikuta akilazimika kuidhinisha hukumu hiyo baada ya BAE System kufikia makubaliano na kitengo cha uchunguzi wa makosa makubwa cha Uingereza, SFO, kuwa kampuni hiyo ikiri kutotunza taarifa za malipo hayo ya siri katika mpango wa ununuzi wa rada ili neno rushwa lisihusishwe kwenye kosa hilo.
BAE System ilikanusha kutumia rushwa katika kuishawishi serikali ya Tanzania kununua rada hiyo kwa bei ya juu na SFO haijaweka neno rushwa kwenye mashtaka yake dhidi ya kampuni hiyo ya Kiingereza, lakini Jaji Bean nusura akwamishe njama hizo baada ya kuhoji sababu za BAE kutoa fedha hizo nyingi kwa Vithlani.
"Siweni kuidhinisha makubaliano haya (baina ya SFO na BAE) hadi nijue malengo ya matumizi ya dola 12.4 za Kimarekani kwa mfanyabiashara wa Tanzania kwa sababu inaonekana kuwa fedha zilikuwa nyingi mno kiasi kwamba angeweza kulipalipa chochote kwa kwa yeyote ambaye angeona ni muhimu katika kufanikisha kushinda zabuni ya dola 40 milioni za Kimarekani," alisema Jaji Bean.
"BAE haikutaka kujua ni kiasi gani cha fedha kingelipwa na kwa nani. Usisikie uovu, usiseme uovu na mambo mengine."
Jaji huyo alisema kuwa kwa maana hiyo kiasi cha fedha alicholipwa Vithlani kingetolewa kwa viongozi wa serikali ili kufanikisha mpango huo.
Lakini katika hukumu ya jana, Jaji Bean pia alikubaliana na maafikiano hayo ya SFO na BAE na kuitaka kampuni hiyo kuilipa Tanzania paundi za 30 milioni za Kiingereza (sawa na Sh63 bilioni) na paundi 225,000 (sawa na Sh472 milioni) za gharama ya kuendesha kesi hiyo.
Kampuni ya BAE ilitakiwa kulipa faini ya Paundi 500,000 kwa kushindwa kuweka taarifa sahihi za malipo ya ununuzi wa rada hiyo katika biashara iliyofanyika mwaka 2007.
Kampuni ya BAE Systems ilimteua raia wa Tanzania Shailesh Vithlani kuwa wakala wa kuisadia kupata zabuni ya kuiuzia Tanzania hiyo ambayo bei yake ilizua gumzo.
Kwa kazi hiyo Vithlani alilipwa Dola za Marekani 12.4 milioni kupitia kampuni moja iliyosajiliwa katika visiwa vya British Virgin vilivyo barani Amerika ya Kusini.
Juzi katika utetezi wake BAE Systems ilisema ilimlipa Vithlani fedha hizo kwa kazi aliyoifanya kuishawishi Tanzania inunue bidhaa hiyo kutoka kwenye kampuni hiyo.
“Kutokana na mazingira halisi ya uuzaji rada kutofuata utaratibu na kukiri kwenu makosa, mahakama inaiamuru BAE kulipa faini ya chinin lakini iilipe Tanzania fedha kwa kiwango cha juu,’’ alisema Jaji Bean.
Wakati kesi hiyo ikiendelea juzi, mjadala mkubwa baina ya upande wa mashtaka na utetezi ulikuwa juu ya matumizi ya fedha hizo zilizolipwa kisiri kwa Vithlani.
Hata hivyo, upande wa utetezi ulisimama imara kupinga kuwa haukufanya malipo yoyote kifisadi ili kufanikisha kupata zabuni hiyo.
Jana Victor Temple wa SFO alliambia mahakama hiyo kuwa BAE imeweka mfumo wa siri na wa wazi wa mawakala watakaofanikishia kampuni hiyo kupata zabuni mbalimbali za kuuza bidhaa zake.
“Kupitia mfumo wa wazi, BAE inafanya kazi zake kwa wazi na wawakilishi wa ofisi hiyo, lakini kwa siri wakala wake hufanya kazi kwa usiri wa hali ya juu kufanikisha malengo yao ya kibiashara,” alisema.
Alisema mwenyekiti wa BAE, Richard Evans alithibitisha kumtumia mfanyabiashara Vithlani katika kufanikisha kampuni hiyo kushinda zabuni ya ununuzi wa rada.
“Uthibitisho huo pia ulitolewa na mjumbe wa bodi ya kampuni hiyo, Mike Turner ambaye baadaye alikuja kuwa mtendaji mkuu wa BAE,” alisema.
Jaji alisema maelezo ya hayo ya utetezi ni tata katika kesi hiyo huku akirudia kumuuliza wakili wa SFO na BAE kuhusu matumizi ya dola 12.4 milioni alizolipwa Vithlani.
Alisema: “Mnapaswa kuonyesha nini kilitokea. Kama hakukuwa na fedha iliyotumika kifisadi, kwa nini ni asilimia 97 ya malipo hayo yalilipwa kupitia kampuni ya BVI inayomilikiwa na kampuni ya BAE kwa kampuni nyingine inayomilikiwa na Vithlani," alihoji.
Wakati Temple alisema kwamba Vithlani aliajiriwa kwa ajili kushawishi zabuni kwa kampuni BAE, jaji huyo alihoji kwa nini mfanyabiashara alilipwa kiasi kikubwa cha fedha?
Temple aliongeza kuwa “kushawishi ni halali, lakini kushawishi ni kitu kingine na ufisadi ni kingine pia".
Habari hii imeandaliwa na Sadick Mtulya na Salim Said kwa msaada wa mashirika ya habari
source. http://www.mwananchi.co.tz/
No comments:
Post a Comment