Viongozi wauziana mashangingi kwa 300,000/-
• Yamo magari ya wahisani yaliyotolewa kama msaada
na Betty Kangonga
WAKATI serikali ikitamba kwamba imejipanga kudhibiti matumizi, baadhi ya vigogo katika wizara na idara mbalimbali wamekuwa wakiuziwa mashangingi ya serikali kwa bei ya sh 300,000 hadi sh milioni mbili, Tanzania Daima Jumatano limebaini!
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa siku kadhaa sasa umebaini magari yaliyouzwa ni yale yaliyokuwa yakitumika kwa miradi ya DFP na ya wizara yaliyotembea kwa zaidi ya kilomita 150,000.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, moja ya wizara ambayo magari yake yameuzwa kwa bei ya kutupwa ni Wizara ya Fedha na Uchumi na majina ya vigogo waliouziwa kwa sasa yamehifadhiwa.
Vyanzo vya habari vilisema magari yaliyouzwa katika wizara hiyo ni yale ya DFP yaliyotolewa na Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
Habari za uhakika kutoka wizara hiyo zinasema magari hayo yamenunuliwa na vigogo wa ndani na nje ya wizara hiyo kwa sh 300,000.
“Magari yote yameuzwa kwa bei ya kutupwa, mimi bosi wangu kanunua moja kwa sh 300,000 eti lilikuwa na tatizo la pump na mengine yaliuzwa kwa sh 500,000 yakiwa mazuri kabisa,” alisema mmoja wa watumishi wa wizara hiyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Mtoaji habari hizo alisema ameamua kupasua bomu hilo kwani anakerwa kuona jinsi serikali inavyoliwa na kuwanufaisha wachache wakati wapo vigogo waliojinunulia zaidi ya magari matatu ya serikali na mengine kuwapa nyumba ndogo zao.
“Wengine tunaagiza magari madogo aina ya Vitz kwa zaidi ya sh milioni sita, lakini shangingi la serikali linauzwa kwa sh 300,000 au 500,000, hii inauma sana,” alisema.
Wakati magari ya Wizara ya Fedha na Uchumi inayooongozwa na Mustafa Mkullo yakiuzwa kwa bei hiyo, magari mengine yaliyouzwa kwa bei chee ni ya Ikulu aina ya Benz, yaliyokuwa yakitumika kwenye misafara ya Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Magari hayo ambayo yanadaiwa kutolewa msaada na serikali ya Cuba, yalibadilishwa na Rais Jakaya Kikwete alipoingia Ikulu na kupata mengine aina ya BMW ambayo pia yalitolewa msaada kwa Tanzania.
Vyanzo vyetu vya habari vilisema kibaya zaidi, baadhi ya magari hayo, yamenunuliwa kwa mkopo na vigogo hao kwa sh milioni mbili.
“Tatizo la yale magari wanasema ni mafuta. Yanakula mafuta vibaya sana, lakini mengine yameuzwa kwa sh milioni mbili na ukitaka naweza kukuelekeza uende mahali linapoegeshwa kalipige picha,” kilisema chanzo chetu kingine cha habari.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uhakiki wa Mali za Umma, Eziera Msanya, alikiri kuwa tatizo la vigogo kujinunulia magari kwa bei poa bila kufuata taratibu lipo na idara yake ambayo ni mpya imejipanga kudhibiti hali hiyo.
Mbali ya kudhibiti tabia ya watendaji kujinunulia magari, Msanya alisema kitengo chake pia kimejipanga kudhibiti matumizi ya magari hayo kwani wapo wanaoyatumia kwa shughuli binafsi kama hata kuyaegesha kwenye vilabu vya starehe.
Alisema utaratibu wa magari ya serikali au mali zozote zile unapaswa kuhakikiwa na kitengo chake na wakiridhika na uhakiki huo na kupanga bei, wanapaswa kutangaza uuzaji wa mali hizo katika mnada wa wazi.
Kabla ya uuzaji wa mali hizo, kitengo chake kinapaswa kupata kibali cha Katibu Mkuu Utumishi ili kuuza mali hizo kwa taratibu zilizowekwa.
“Lakini badala yake watu hawafuati taratibu, siasa zimeingia kati, mtu anaona gari hili linataka kuuzwa, anamwendea waziri husika na kuomba auziwe gari, jambo ambalo ni kinyume kabisa na utaratibu,” alisema Msanya.
Alisema kitengo chake kiko chini ya Wizara ya Fedha na ndicho chenye dhamana ya kuhakiki mali za umma na kutoa mapendekezo ya kuuzwa sambamba na bei zake.
“Unajua hili swala liko kisiasa zaidi na sisi kama ofisi ya uhakiki wa mali za serikali ikitoa maelekezo, hayatekelezwi na hapo ndipo wanapouziana kwa bei poa. Hata hivyo Msanya alilitaka gazeti hili kwenda Wizara ya Uchimi na Fedha kupata ufafanuzi wa magari ya DFP yaliyouzwa hivi karibuni kwa bei ya kutupwa.
Tanzania Daima Jumatano ilipofika wizarani, ilikutana na ofisa habari msaidizi wa wizara hiyo, Ramadhan Mohamed, ambaye alimtaka mwandishi kuacha maswali ili yajibiwe na wahusika kwani alikiri kuwa hakuwa na uwezo wa kuyajibu.
Hata baada ya kuacha maswali hayo, maafisa wa wizarani hapo, akiwemo Waziri Mkulo na Naibu Katibu Mkuu wake, John Haule, walikutana kwa dharula kwa zaidi ya saa tatu ili kutolea ufafanuzi suala hilo.
Akizungumzia uuzwaji wa magari hayo kwa vigogo, Haule alisema upo utaratibu unaotumika katika kuuzia vigogo magari hayo ikiwemo kujua muda wa mkataba wa magari hayo.
Alisema baada ya kupata kibali cha kuuza magari toka mamlaka husika, hupeleka kibali hicho katika ofisi ya Katibu Mkuu Utumishi na kupata kibali cha kuuza magari hayo.
“Ili gari la serikali liuzwe, linapaswa liwe limetembea kilometa kati ya 150,000 hadi 200,000 na lazima liwe limetumika ndani ya miaka mitano, kwa hiyo kama yapo yaliyouzwa basi yalikuwa yameshatumika kwa mujibu wa utaratibu wa magari ya Serikali.
source:http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=22170
No comments:
Post a Comment