Pages

Tuesday, December 21, 2010

Hoseah amlipua Kikwete


• Asema anaogopa kushughulikia ufisadi wa vigogo





na Edward Kinabo









MTANDAO wa Wikileaks wa Marekani umeibua siri nzito kuhusu uwezo na nia ya Rais Jakaya Kikwete katika kushughulikia ufisadi, ukidai kuwa ndiye anayekwamisha kushtakiwa kwa baadhi ya vigogo serikalini wanaotuhumiwa kuhusika katika rushwa kubwa nchini.

Katika taarifa hiyo iliyochapishwa jana na gazeti la The Guardian la Uingereza, likinuu taarifa za kibalozi za Marekani zilizoanikwa na Wikileaks, lilisema Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea, alimweleza mwanadiplomasia mmoja wa Kimarekani kwamba ugumu wa kupambana na ufisadi Tanzania unaanzia Ikulu.



Mtandao huo ulinukuu baadhi ya maelezo ya faragha kuhusu rushwa aliyoyatoa Dk. Hosea kwa mwanadiplomasia wa Kimarekani aitwaye Purnell Delly, walipokutana mwezi Julai mwaka 2007, Dar es Salaam.



Likinukuu mtandao huo, The Guardian liliandika, “Dk. Hosea alidokeza kuwa Rais Kikwete hafurahishwi na sheria kuchukua mkondo wake dhidi ya ufisadi ambao unaweza kuwatia hatiani vigogo wa ngazi za juu serikalini…. Hataki kuweka msingi wa kumwandama kiongozi yeyote miongoni mwa watangulizi wake (wastaafu).”



Linasema mwanadiplomasia huyo alisema: “Hosea alikuwa akisisitiza kwamba akiamua kuwa na makali, usalama wake binafsi utakuwa hatarini…anadai anaamini maisha yake yako hatarini, kwani amekuwa akipokea ujumbe wa vitisho kwa simu na barua na amekuwa akikumbushwa kila siku kwamba anapambana na ‘watu matajiri na wenye nguvu.’”



Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dk. Hosea alitoa maelezo yanayokatisha tamaa juu ya mustakabali wa mapambano dhidi ya ufisadi nchini na ugumu uliopo katika kuwashtaki watuhumiwa wa ufisadi mkubwa.



“Alituambia bila kufafanua... kwamba kesi zinazomhusu waziri mkuu au rais haziwezi kujadiliwa kabisa,” kilisema chombo hicho na kisha kufafanua: “Rais Kikwete hataki kumshughulikia mtangulizi wake yeyote mwenye tuhuma zinazostahili kufikishwa mahakamani.”



Dk. Hoseah anadaiwa kumueleza mwanadiplomasia huyo jinsi rushwa ilivyokithiri katika Benki Kuu ya Tanzania na visiwani Zanzibar, lakini akadokeza ugumu wa kuishughulikia kwa sababu tu wahusika wakuu ni watu ambao “hawahusiki”.



Hoseah alidokeza kuwa mambo yakiwa mabaya angeweza hata kukimbia nchi, kwa mujibu wa taarifa hiyo ikimnukuu mwanadiplomasia huyo wa Marekani.



“Ukihudhuria kwenye vikao vya juu (vya ndani), watu wanataka ujisikie kuwa wao ndio wamekuweka hapo ulipo. Wakiona huenendi na yale wanayotaka wao, basi hapo unakuwa katika hatari,” ilisema sehemu nyingine ya taarifa hiyo ikinukuu maelezo ya Dk. Hoseah.



Aidha, katika mazungumzo yao, Dk. Hoseah alimpa matumaini mwanadiplomasia huyo kwamba TAKUKURU ingeweza kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wote waliohusika katika kile alichokiita ‘dili chafu’ ya rushwa katika ununuzi wa rada ya kijeshi kutoka kampuni ya BAE ya Uingereza, hatua ambayo hata hivyo ilionekana isingeweza kutekelezwa na taasisi hiyo.



Wachambuzi wa mambo wanasema kauli hiyo ya Dk. Hoseah ilitokana na ukweli kwamba tayari wapelelezi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai ya Uingereza (SFO) walikuwa wameshampelekea faili lote la watuhumiwa likiwa na ushahidi jambo ambalo lingeweza kumuepusha na hatari ambayo ingeweza kumfika kama uchunguzi huo ungefanywa na TAKUKURU yake.



Katika kashfa hiyo, serikali ya Tanzania inadaiwa kununua rada ya kuongozea ndege za kiraia na za kivita kutoka kampuni ya BAE System ya Uingereza kwa gharama kubwa ya dola 40 milioni, huku taarifa za uchunguzi kutoka SFO na vyanzo mbalimbali zikionyesha kuwa ununuzi huo haukuwa wa lazima na uligubikwa na rushwa.



Kashfa ya rada ilitendeka mwaka 1999, katika mazingira yaliyogubikwa na rushwa kwa watendaji serikalini ili waweze kulainisha watoa maamuzi. Kwa mujibu wa taarifa za maelezo ya Dk. Hoseah kwa mwanadiplomasia huyo, watuhumiwa zaidi wa rushwa ya rada wapo katika Wizara ya Ulinzi na jeshini.



“Dk. Hoseah aliliita suala la rada kuwa ni dili chafu na kusema inawahusu maofisa wa Wizara ya Ulinzi na vigogo wawili au mmoja wa jeshi (hawakutajwa majina),” ilieleza taarifa hiyo.



Kesi ya rada iliendelea kusikilizwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini London, Uingereza.









source:freemedia.co.tz

No comments: